Lugha Nyingine
Maonyesho ya Uchumi na Biashara?ya China na Afrika yapata ushiriki wa juu zaidi
Watazamaji wakipiga picha pamoja kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonyesho cha Changsha wakati wa Maonyesho ya Tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika huko Changsha, Mkoa wa Hunan, katikati mwa China, Julai 1, 2023. (Xinhua/Chen Yehua) |
CHANGSHA - Maonyesho ya Tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika yamefungwa Jumapili, huku miradi 120 yenye thamani ya jumla ya dola za Marekani bilioni 10.3 ikitiwa saini, maofisa wa Serikali ya China wamesema.
Maonyesho hayo yaliyofanyika kwa siku nne yalianzia Alhamisi wiki iliyopita huko Changsha, mji mkuu wa Mkoa wa Hunan katikati mwa China. Hunan ni moja ya mikoa ya China yenye shughuli nyingi zaidi katika uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na Afrika.
Yakiwa na wageni kutoka nje ya China 1,700 na zaidi ya watembeleaji 10,000 wa ndani ya China, ushiriki katika maonyesho ya mwaka huu umekuwa wa kiwango cha juu kabisa, amesema Zhou Yixiang, naibu katibu mkuu wa serikali ya Mkoa wa Hunan.
Idadi ya kampuni na wajasiriamali walioshiriki kwenye maonyesho hayo na idadi ya bidhaa na huduma zilizoonyeshwa za Afrika zimeshuhudia viwango vya juu vya kihistoria, huku takwimu zikiongezeka kwa asilimia 70 na asilimia 166 kuliko maonyesho yaliyopita, amesema Shen Yumou, mkuu wa idara ya biashara ya Hunan.
Shen amesema, nchi zote 53 za Afrika ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia na China zimeshiriki kwenye maonesho hayo, ambapo mashirika 12 ya kimataifa, wafanyabiashara wa China na Afrika, mashirika ya wafanyabiashara, mashirikisho ya wafanyabiashara na taasisi za kifedha zaidi ya 1,700 zimeonesha bidhaa zao mbalimbali kwenye maonesho hayo.
"Inadhihirisha uhai na uhimilivu wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika," amesema.
China ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Bara la Afrika na chanzo chake cha nne kwa ukubwa duniani cha uwekezaji. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa biashara kati ya China na Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 282 Mwaka 2022. Katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huu, uwekezaji mpya wa moja kwa moja wa China (FDIs) barani Afrika ulifikia dola bilioni 1.38, ikiwa ni ongezeko la asilimia 24 kuliko mwaka uliopita.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma