Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping akutana na mwenzake wa Indonesia Joko Widodo mjini Chengdu
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Rais wa Indonesia Joko Widodo huko Chengdu, Mji Mkuu wa Mkoa wa Sichuan, Kusini-Magharibi mwa China, Julai 27, 2023. Rais Widodo yuko Chengdu kushiriki kwenye ufunguzi wa Michezo ya 31 ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Duniani (FISU) ya majira ya joto ya Chengdu na kufanya ziara China. (Xinhua/Yin Bogu)
CHENGDU - Rais Xi Jinping wa China amekutana na Rais wa Indonesia Joko Widodo huko Chengdu, Mji Mkuu wa Mkoa wa Sichuan, Kusini Magharibi mwa China ambaye yuko hapa kushiriki kwenye ufunguzi wa Michezo ya 31 ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Duniani (FISU) ya majira ya joto ya Chengdu na kufanya ziara China.
Kwenye mazungumzo yao yaliyofanyika Alhamisi, Rais Xi amesema, mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa ushirikiano wa kiwenzi wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Indonesia. Amesema, China iko tayari kutumia fursa hii kuendeleza kwa kina ushirikiano wa kimkakati na Indonesia, kuweka mfano kwa nchi zinazoendelea wa kuchangia mustakabali wa pamoja, kutafuta mshikamano na ushirikiano na kuhimiza maendeleo ya pamoja, na kuingiza uhakika na nishati chanya zaidi katika kanda na Dunia.
Amesema, China iko tayari kudumisha mawasiliano ya kimkakati ya mara kwa mara na Indonesia, kuimarisha mabadilishano ya uzoefu wa uongozi wa serikali, kuanzisha utaratibu wa mazungumzo ya "2+2" kwa mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa nchi hizo mbili, na kujenga kuaminiana kimkakati kwa ngazi ya juu.
“Mafanikio makubwa yamepatikana katika kuunganisha Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na Dira ya Indonesia ya Egeo la Kimataifa la Bahari,” Rais Xi amesema huku akiitaja Reli ya Mwendo kasi ya Jakarta-Bandung ambayo itaanza kutumika hivi karibuni kama mfano.
Rais Xi ameeleza kuwa China iko tayari kuimarisha mawasiliano na uratibu na Indonesia chini ya Kundi la 20 (G20), BRICS, Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini Mashariki (ASEAN) na mifumo mingine ya kimataifa, kuhimiza utekelezaji wa Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Usalama wa Dunia na Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia, kulinda amani na utulivu wa kikanda na kimataifa, na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.
Kwa upande wake Widodo, amesisitiza kuwa Indonesia inashikilia sera ya kuwepo kwa China moja, amesema uhusiano wa nchi hizo mbili umepata maendeleo makubwa tangu alipompokea Rais Xi huko Bali mwaka jana.
Amesema nchi yake iko tayari kuimarisha ushirikiano na China katika uwekezaji, uvuvi wa baharini, usalama wa chakula na afya huku akieleza kuwa Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Usalama wa Dunia na Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia yaliyotolewa na Rais Xi ni wazi na jumuishi na Indonesia inaunga mkono juhudi hizo.
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Rais wa Indonesia Joko Widodo huko Chengdu, Mji Mkuu wa Mkoa wa Sichuan, Kusini-Magharibi mwa China, Julai 27, 2023. (Xinhua/Ding Haitao)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma