Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping ahimiza China na Afrika kuungana mkono kwa ajili ya maendeleo ya kisasa
Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba kwenye Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Agosti 24, 2023. Rais Xi ameongoza kwa pamoja na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika Alhamisi. (Xinhua/Huang Jingwen)
JOHANNESBURG - Rais Xi Jinping wa China ametoa hotuba muhimu kwenye Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika na kuzihimiza China na Afrika kuungana mikono kwa ajili ya maendeleo ya kisasa.
Kwenye hotuba yake hiyo siku ya Alhamisi, Rais Xi amesema China iko tayari kuanzisha Mpango wa Kusaidia Maendeleo ya Viwanda barani Afrika, ambao utasaidia Afrika katika kukuza sekta yake ya viwanda na kufikia ukuaji wa viwanda na uchumi mseto.
Mpango huo umesisitiza kuwa kupitia miradi tisa iliyo chini ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na Mpango wa Maendeleo wa Dunia, China itaelekeza rasilimali zaidi za misaada, uwekezaji na ufadhili kwenye programu za uanzishaji wa viwanda.
“China itaanzisha Mpango wa China Kusaidia Uboreshaji wa Kilimo wa kisasa wa Afrika,” Rais Xi amesema, huku akiongeza kuwa China itaisaidia Afrika kupanua mashamba ya nafaka na kuhimiza kampuni za China kuongeza uwekezaji wa kilimo barani Afrika.
Mpango huo unalenga kusaidia Afrika kufikia kujitosheleza kwa chakula na maendeleo endelevu ya kujitegemea, kukuza uzalishaji wa chakula barani Afrika, kuimarisha kwa ufanisi uwezo wa Afrika wa kulinda usalama wake wa chakula, na kuisaidia kufikia malengo husika katika kukifanya kilimo kuwa cha kisasa.
China itakuwa mwenyeji wa Kongamano la pili la Ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika huko Hainan mwezi Novemba mwaka huu, amesema Rais Xi, na kuongeza kuwa China itatoa msaada wa dharura wa chakula kwa baadhi ya nchi za Afrika zinazohitaji ili kusaidia Afrika kukabiliana na athari za sasa za chakula.
“China pia itaanzisha mpango wa Ushirikiano kati ya China na Afrika katika kuwaandaa watu wenye ujuzi, ikipanga kutoa mafunzo kwa wakuu na walimu 500 wa vyuo vya ufundi stadi, na wafanyakazi 10,000 wenye ujuzi wa lugha ya Kichina na ufundi stadi kwa ajili ya Afrika kila mwaka,” Rais Xi amesema.
Mwaka 2013, Rais Xi alitangaza kanuni ya ukweli, uhalisi, karibu na udhati kwenye sera ya China kuhusu Afrika. "Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, China imeendelea kujitolea kwa kanuni hii," Rais Xi amesema.
Rais Xi ametoa wito kwa China na Afrika kushirikiana pamoja ili kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya kutimiza mitazamo yao ya maendeleo kwa kuhimiza utaratibu wenye haki na usawa wa kimataifa, kufuata msimamo wa ushirikiano wa kweli wa pande nyingi na kupinga kithabiti madhara ya ukoloni na umwamba wa aina zote.
Rais Xi Jinping wa China akiongoza kwa pamoja na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika, mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Agosti 24, 2023 Alhamisi. (Xinhua/Zhai Jianlan)
Rais Xi Jinping wa China akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika, mjini Johannesburg, Afrika Kusini, Agosti 24, 2023 Alhamisi. (Xinhua/Huang Jingwen)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma