Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping na mwenzake Joe Biden wafanya mazungumzo kwa njia ya simu
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amezungumza na Rais wa Marekani Joe Biden kwa njia ya simu siku ya Jumanne kwa ombi la rais huyo. Marais hao wawili wamekuwa na mazungumzo ya wazi na ya kina kuhusu uhusiano wa China na Marekani na masuala mengine yanayohusu maslahi kwa pande zote.
Rais Xi ameeleza kuwa mkutano wake wa San Francisco na Rais Biden Novemba mwaka jana ulifungua matarajio ya San Francisco ya kuelekea siku za baadaye na kwamba katika miezi iliyopita, maofisa viongozi wa pande mbili wamechukua hatua na kuzitekeleza kwa makini kwa kufuata maelewano ya marais hao wawili, hali ambayo imefanya uhusiano wa China na Marekani kuanza kuwa na mwelekeo wa utulivu, na hii inakaribishwa na sekta mbalimbali za nchi hizi mbili na jumuiya ya kimataifa. Amesema, kwa upande mwingine, mambo hasi ya uhusiano huo pia yamekuwa yakiongezeka, na hii inahitaji tahadhari kutoka kwa pande zote mbili.
Rais Xi amesisitiza kuwa suala la uelewa wa kimkakati siku zote ni la msingi kwa uhusiano wa China na Marekani, kama kifungo cha kwanza cha shati ambacho lazima kiwekwe sawa. Amesema, nchi mbili kubwa kama zilivyo China na Marekani hazipaswi kukata mawasiliano kati yao au kugeuziana kisogo, na zinapaswa kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na kutafuta ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote.
Rais Xi amebainisha kanuni kuu tatu zinazopaswa kuongoza uhusiano wa China na Marekani Mwaka 2024. Kwanza, amani lazima ithaminiwe, pili, utulivu lazima upewe kipaumbele, na tatu, kuaminika lazima kudumishwe. Amesema pande hizo mbili zinapaswa kuheshimu ahadi zao kwa kila mmoja kwa vitendo, na kubadilisha matarajio ya San Francisco kuwa hali halisi.
Rais Xi amesisitiza kuwa suala la Taiwan ni mstari mwekundu wa kwanza ambao haupaswi kuvukwa katika uhusiano wa China na Marekani. Amesema, katika kukabiliana na makundi yanayofanya shughuli ya mafarakano za kuifanya "Taiwan ijitenge" na kupigwa jeki na kuungwa mkono kutoka nguvu ya nje kwa makundi hayo, China haitakaa kimya na kufunga mikono yake.
Rais Xi amesema, upande wa Marekani umepitisha msururu wa hatua za kukandamiza maendeleo ya biashara na teknolojia ya China, na inaongeza kuyawekea mashirika zaidi na zaidi ya China kwenye orodha yake ya vikwazo. Amesema, hii siyo "kuondoa hatari," bali ni kutengeneza hatari.
Rais Xi ameeleza msimamo wa China kuhusu masuala yanayohusu Hong Kong, haki za binadamu, na Bahari ya Kusini.
Rais Biden amesema kuwa uhusiano wa Marekani na China ndiyo uhusiano wa pande mbili wenye ushawishi mkubwa na wa kina zaidi duniani na kwamba maendeleo katika uhusiano huo tangu kufanyike mkutano wa San Francisco yanaonyesha kwamba pande hizo mbili zinaweza kuendeleza ushirikiano huku zikisimamia tofauti kwa kuwajibika. Rais Biden amesema, anasisitiza tena kwamba Marekani haitafuti Vita Baridi vipya, haitafuti kubadili mfumo wa China, haitafuti kupinga China kwa kupitia kuimarisha uhusiano wa nchi zilizo kwenye itifaiki yake, Marekani haiungi mkono "Taiwan ijitenge," na Marekani haina nia ya kufanya mgogoro na China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma