Lugha Nyingine
Mavazi kwenye matairi: Maduka yanayotembea yaongezeka Zimbabwe kutokana na ugumu wa maisha
Katika makutano ya barabara yenye shughuli nyingi katika Mji Mkuu wa Zimbabwe, Harare, muuzaji bidhaa anazungumza na mteja ambaye kwa umakini mkubwa anatazama suruali zinazouzwa kutoka kwenye duka linalotembea pembezoni mwa barabara.
Mazungumzo yaliendelea kwa muda kiasi wakati mteja huyo akijitahidi kupunguza bei na muuzaji akimshawishi mteja wake kununua bidhaa.
Mwishowe, mteja anaonekana kurizika, kamkabidhi muuzaji noti ya dola 10 za kimarekani, akafungasha suruali katika begi lake na kuondoka kutoka barabara yenye watu wengi.
Mmiliki wa duka hilo linalotembea aitwaye Gift Makombe mwenye umri wa miaka 55 amekuwa akiuza zaidi nguo za mtumba za wanaume kwa kutumia gari lake kwa zaidi ya muongo na amefanikiwa sana katika kushawishi wateja.
Baada ya kushindwa kupata ajira rasmi kufuatia kufungwa kwa kampuni ya ulinzi aliyokuwa akifanya kazi ya ulinzi kwa miongo mbili, Makombe aliamua kuanzisha biashara hiyo ya kutembeza mitaani.
“Niliamua kuwa mchuuzi kufuatia kufungwa kwa kampuni ya ulinzi niliyokuwa nafanya kazi. Nilienda kijijini baadaye nikarudi mjini, nikakopa fedha ili niweze kuanzisha biashara.” Makombe aliliambia Shirika la Habari la Xinhua.
Kupitia biashara hiyo ya kutembeza mavazi mitaani, baba huyu mwenye watoto watano ameweza kupeleka watoto wake shuleni na kusaidia familia yake iliyopo kijijini. Hata hivyo, alisema kwamba kama mazingira yangeruhusu angechagua kazi rasmi badala ya uchuuzi wa bidhaa mitaani.
“Kupata kazi ya kudumu kunalipa, lakini kupata ajira kwenye makampuni ilikuwa vigumu maana makampuni mengi yalikuwa hayatoi ajira. Kwa hivyo niliamua kufanya biashara ya mitaani ili niweze kutunza familia yangu. Kama nikifanikiwa kupata dola za kimarekani 10 kwa siku nitatuma kiasi kijijini, familia yangu inaweza kuishi na hii inaniwezesha kwenda kuwatembelea na baadaye kurudi mjini.” anasema.
Licha ya kuwa na leseni ya kufanya biashara, Makombe anasema mara kadhaa wauzaji bidhaa mitaani wamajikuta katika mapambano na watekelezaji wa sheria ambao wanawashutumu kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Maduka yanayotembea yamekuwa maarufu nchini Zimbabwe baada ya janga la UVIKO-19 kuwafanya watu wengi kupoteza ajira rasmi na hivyo kuingia katika biashara zisizo rasmi.
Baada ya kufanya kazi kwa miaka 10 na bado akashindwa kukidhi mahitaji ya kila siku, Rodreck Limula aliamua kuanzisha biashara inayotembea.
Alisema kushindwa kulipa kodi ya pango katika eneo la biashara katikati ya mji wa Harare kulimfanya kuanzisha biashara hiyo ya kutembeza bidhaa bila changuo lingine.
“Tuligundua kwamba biashara ya kutembeza bidhaa ni bora zaidi kuliko kupanga pango kwa ajili ya biashara, kwa sababu kodi ni kubwa. Zaidi kuna watu wengi wanapita kwenye mitaa, hivyo tunakutana na watu wa aina tofauti na hivi ndivyo tunafanya biashara.” alisema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma