Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping afanya mazungumzo na Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune
Rais wa China Xi Jinping amefanya mazungumzo siku ya Jumanne na Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, China.
Rais Xi amesema kuwa mwaka huu inatimia miaka 65 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Algeria, katika miaka 65 iliyopita, China na Algeria zilikuwa katika juhudi za pamoja kwa kutimiza lengo kuu la pamoja la kupinga ubeberu na ukoloni na kutafuta uhuru na ukombozi wa kitaifa.
"Wakati China inaendeleza ustawishaji wa kitaifa katika mambo yote kupitia njia ya maendeleo ya kisasa ya China, Algeria inasonga mbele kujenga 'Algeria mpya.' China itashirikiana na Algeria kuendeleza urafiki wa muda mrefu na kufanya jitihada katika kutafuta maendeleo makubwa zaidi kwenye ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Algeria," Rais Xi amesema.
Amesisitiza umuhimu wa pande hizo mbili kusaidiana katika masuala ya maslahi ya msingi. Ameishukuru Algeria kwa uungaji mkono wake wa dhati kwa msimamo wa haki wa China katika masuala yanayohusiana na Taiwan, Xinjiang na haki za binadamu, na amesisitiza kwamba China inaiunga mkono kithabiti Algeria katika kulinda mamlaka ya nchi, uhuru na ukamilifu wa ardhi, inaunga mkono Algeria kufuata njia ya maendeleo inayoendana na hali halisi ya nchi yake , na inapinga uingiliaji wa nje katika masuala ya ndani ya Algeria.
Rais Xi amesema, pande hizo mbili zinahitaji kushirikiana pamoja katika utekelezaji wa nyaraka muhimu za Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na ushirikiano mwingine, kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya jadi kama vile miundombinu, mafuta ya petroli, madini na kilimo, na kupanua ushirikiano katika nyanja za teknolojia ya juu ikiwa ni pamoja na safari kwenye anga ya juu, nishati ya nyuklia, TEHAMA na nishati mbadala ili kukuza vichocheo vipya vya ukuaji wa ushirikiano.
“Mwaka huu inatimia miaka 60 tangu China kutuma timu yake ya kwanza ya madaktari nchini Algeria. Katika miongo sita iliyopita, wahudumu wa afya wa China 3,522 wametumwa Algeria, kutibu zaidi ya watu milioni 27 na kusaidia akina mama kujifungua watoto zaidi ya milioni 2.07. "Hii ni alama ya kihistoria kwa urafiki kati ya China na Algeria," Rais Xi amesema.
Rais wa China ameeleza utayari wa China kushirikiana na Algeria ili kuharakisha utekelezaji wa matokeo ya mkutano wa kwanza wa viongozi wakuu wa China na nchi za Kiarabu na kuimarisha ushirikiano chini ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Kwa upande wake Tebboune amesema kuwa China ni rafiki na mshirika muhimu zaidi wa Algeria. Ameishukuru China kwa kuipa Algeria uungwaji mkono wa aina mbalimbali kwa miaka mingi, akisema Algeria inaunga mkono kithabiti msimamo wa China kuhusu masuala ya Taiwan na Xinjiang yanayohusiana na maslahi makuu ya China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma