Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping atoa wito kwa China na Afrika Kusini kuimarisha ushirikiano wa ngazi nne katika enzi ya dhahabu
Rais Xi Jinping wa China na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wakifanya mazungumzo mjini Pretoria, Afrika Kusini, Agosti 22, 2023. (Xinhua/Yin Bogu) |
PRETORIA - Rais Xi Jinping wa China ametoa wito kwa China na Afrika Kusini kuimarisha ushirikiano wao wa ngazi nne kwenye ziara yake ya kitaifa nchini Afrika Kusini.
Rais Xi ametoa wito huo siku ya Jumanne wakati alipofanya mazungumzo na mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, hapa Pretoria.
Kabla ya kuwasili kwake nchini humo, Rais Xi alisema katika makala yake iliyochapishwa na vyombo vya habari vya Afrika Kusini kwamba uhusiano unaostawi kati ya China na Afrika Kusini "umeingia katika 'zama ya dhahabu,' yenye matarajio mapana na mustakabali wenye matumaini."
Kwenye mazungumzo hayo, rais Xi ametoa wito kwa pande zote mbili kuwa wenzi wa kimkakati wa kuaminiana kwa kiwango cha juu, akiongeza kuwa "urafiki na undugu" ndiyo ubora wa kweli wa uhusiano kati ya pande mbili.
Amesema, pande hizo mbili zinapaswa kuimarisha mabadilishano na ushirikiano kati ya mabunge yao, vyama vya siasa, wanajeshi na serikali za mitaa, na kuendelea kusaidiana katika masuala yanayohusu maslahi ya kimsingi ya kila mmoja na mambo yanayofuatiliwa kwa pamoja.
Ameelezea kunufaishana ni alama ya ushirikiano kati ya China na Afrika Kusini, akisema kwamba pande hizo mbili zinapaswa kutilia maanani kuendeleza Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja, kutekeleza mipango tisa yaliyowekwa kwenye baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, pamoja na Mpango Mkakati wa Miaka 10 wa Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, kuimarisha ushirikiano katika maeneo yenye nguvu na kuhimiza maeneo mapya ya ukuaji wa ushirikiano.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa biashara kati ya nchi hizo mbili Mwaka 2022 ilifikia dola za kimarekani bilioni 56.74, ikichukua asilimia 20.1 ya jumla ya biashara kati ya China na Afrika. Na katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia dola bilioni 28.25, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.7 mwaka jana wakati kama huo.
China inaendelea kuwa mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika Kusini kwa miaka 14 mfululizo, huku Afrika Kusini ikiwa mwenzi mkubwa wa kibiashara wa China barani Afrika kwa miaka 13 mfululizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo, pande hizo mbili pia zimeahidi kuendelea kutafuta uimarishaji wa ushirikiano katika maeneo muhimu kama vile miundombinu na uchukuzi, biashara na uwekezaji, viwanda, usindikaji wa mazao ya kilimo, nishati na rasilimali, sekta ya fedha, uchumi wa kidijitali, sayansi na teknolojia na maendeleo ya kijani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma