Lugha Nyingine
Rais wa Indonesia afanya safari ya majaribio ya ART huko Nusantara, mji mkuu mpya
NUSANTARA - Rais wa Indonesia Joko Widodo Jumanne amefanya safari ya majaribio ya reli ya kiotomatiki ya mfumo wa usafiri wa haraka (ART) uliotengenezwa na China katika mji mkuu mpya Nusantara wa nchi hiyo ya Asia Kusini-Mashariki, siku ya Jumanne. Mfumo huo wa ART ni mradi wa ushirikiano kati ya Kundi la Kampuni za CRRC la China na Kampuni ya Kimataifa ya NORINCO, kwa sasa uko katika hatua ya uendeshaji wa majaribio.
Mapema ya siku hiyo, wakati akizungumza na magavana, mameya, na maofisa katika mkutano huko Nusantara, Widodo alilinganisha gharama kati ya ART na mifumo ya reli ya kawaida, akibainisha kuwa mfumo wa ART ni nafuu zaidi.
Amefafanua kuwa, "Kwa hili, usafiri wa reli ya kiotomatiki hakika ni wa bei nafuu kwa sababu hauhitaji reli, unatumia sumaku. Kwa kila treni kwa mabehewa matatu, bei ni rupiah bilioni 74 hivi (dola za Kimarekani karibu milioni 4.7)," na pia amelinganisha huduma hiyo na kupanda kwa gharama kwa mifumo ya Usafiri wa Haraka wa Umma na Usafiri wa Reli Nyepesi.
Ameelezea imani yake kuwa mfumo ART unaweza kuleta njia mbadala endelevu na ya gharama nafuu kwa mifumo ya kawaida ya reli nchini Indonesia, hasa katika miji ambayo inazidi kuwa na msongamano.
"Mfumo wa ART ni kiwakilishi cha mafanikio ya teknolojia ya hali ya juu ya China na tayari umefanyiwa mipango ya kibiashara katika miji kadhaa ya China na Abu Dhabi katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Tutaendelea kujikita katika kutembeza mfumo huo nchini Indonesia na masoko mengine ya kimataifa, ili kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya usafiri wa kijani duniani,” amesema Wang Xiaobing, naibu mkuu wa NORINCO.
Wizara ya Mawasiliano ya Indonesia itafanya majaribio ya ufundi na tathmini za kina, na kampuni husika za mradi huo zitafanya uboreshaji unaohitajika kulingana na matokeo ili kuhakikisha uendeshaji mzuri wa mfumo huo nchini Indonesia.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma